Friday, July 6, 2012

Mgomo wa Mabasi ya Abiria Mjini Moshi

 Wakazi wa Manispaa ya Moshi na vitongoji vyake leo wameonja adha ya kukosa usafiri kufuatia mgomo wa mabasi  yanayotoa huduma ya usafiri mjini hapa, maarufu kama daladala.


 Kituo kikuu cha Mabasi mjini Moshi kama inavyoonekana dakika chache zilizopita

 Mgomo huo umetokea kama hatua za waendeshaji wa huduma hiyo kupinga kupanda kwa kiwango cha ushuru kilichotangazwa na Halmashauri ya Manispaa hiyo.

Vibao vipo, magari hayaonekani

 Kwa  mujibu wa tangazo la Halmashauri hiyo inayoongozwa na CHADEMA, ushuru huo umepanda kwa asilimia 50 kutoka Tsh. 1000 zilizokuwa zikilipwa awali mpaka Tsh 1500 zinazotakiwa kuanza kulipwa mara moja.

Kituo kikiwa tupu, huku Polisi wa 'kutuliza' ghasia wakiwa kazini
Tayari Katibu wa CHADEMA mkoani Kilimanjaro, Bw. Lema, kupitia Radio za FM mjini hapa ametoa tamko la kupinga vikali ongezeko hilo, akiliita kuwa 'hujuma' inayofanywa na baadhi ya watendaji wa Halmashauri hiyo inayoongozwa na chama chake kuonyesha kuwa kimeshindwa kazi.

Tuesday, June 12, 2012

Blogging Revolution: Shubiri kwa wajiitao serikali


Kitabu kizuri kinachoangazia mabadiliko ya kijamii na kisiasa yaliyoletwa na matumizi ya zana za uandishi wa kiraia hususani blogu.

 Kinatazama namna blogu zilivyochangia Mapinduzi yanayoendelea katika nchi za kiarabu –maarufu kama Arab Spring – na jinsi ambavyo blogu hizi zinaanza kuwatia hofu watu wanaojiita serikali.

Sunday, May 20, 2012

Umemsoma Dambisa Moyo?


Kama una mpango wa kusoma kitabu kimoja tu mwaka huu, napendekeza hiki cha Dambisa Moyo kiitwacho "How the West was Lost". Ukikisoma utaelewa zaidi kwa nini hawa watawala wanaoitwa "The darling of the west" wanaopigana vikumbo kuhudhuria mkutano wa G8, wamepotea njia. Anacho kingine alichokiandika kabla ya hiki, kiitwacho cha Dead End, bado nakitafuta. Naambiwa ni moto.

Saturday, May 19, 2012

Mafanikio ni umiliki wa muda wako



Mafanikio ni nini?
Ajira ya uhakika?
Uhakika wa mapato?
Uhakika wa pensheni?
Ongezeko la muamala mwisho wa mwezi?
Tarakimu za shilingi kuongezeka?
Kwa gharama ya kunyang'anywa muda wako?
Si unajua?
Kadri ziongezekavyo ndivyo uuzavyo muda wako?



Mafanikio....
Ni madaraka kazini?
Madaraka yaendanayo na ubize?
Kutwa u ziarani? U angani kikazi?
Waondoka alfajiri, warudi usiku?
Wanao hawakuoni?
Mwenza yu mpweke?
Haidhuru...
Nyumba yanukia noti sio?
Shilingi bila muda, kazi yake nini?

Muda na familia ni sehemu ya mafanikio. Noti ziendazo sambamba na kukunyang'anya fursa hii, faida yake nini? |Picha ya blackmarriageworks.com/







Mafanikio...
Ni kuongezeka kwa kibaba?
Ankara zalipika kibaba kinabaki?
Ni uhuru wa muda wako?
Uhuru wa kujenga familia kwa karibu?
Mwenzi achekelee? Wana wasome?
Uifaidie jamii?
Sadaka utoe?
Wenye shida wakukimbilie?



Si unajua lakini...?
Bila shilingi hayo si mepesi?
Shilingi yatatua vingi
Muda bila shilingi, wa nini?
Muda unao unachotatua hakionekani?
Na wadai umefanikiwa? Kivipi?


Hujanielewa...
Mafanikio ni kuwa na vyote
Ni thamani ya muda wako
Hiari ya matumizi ya muda wako
Mafanikio ni...
Mfumo ukutumikiao wewe
Mfumo ukupao muda wako wote
Si tu kulipa ankara kwa kutumikia shilingi
Bali...
Shilingi zakutumikia wewe
Na uhuru KAMILI wa muda wako uwe nao

Nauliza umefanikiwa?
Kazana kutengeneza mfumo
Usitumikie mfumo

Friday, May 18, 2012

Nani yu huru?

Wakurupuka alfajiri, haraka wende kazini
Wajutia kuliacha shuka, waogopa kuchelewa
Ukifanyacho kimepangwa, mpangaji ni mwajiri
Muda ulohisi wako, ukweli si wako
Mwajiri kaununua nira kakufungia
Wajisifu na ajira?

Mwajiriwa akilinda kibarua chake|Picha ya picturesof.net
                                     


















Uhuru ni nini na aliye huru ni nani?
Aliyehuru hufugwa na mwingine, ati?
Aliye huru yuna muda
Cha kufanya akipanga yeye, pa kwenda haamrishwi
Huenda atakako kwa hiari ya muda wake
Hupata mkate wake pasipo mauzo ya muda wake
U huru?


Mtumwa aongozwa na bwana wake
Hiari na aendako hanayo
Kazini ni lazima
Ujira huupata kwa kuuza uhuru wake
Hana mamlaka na muda alodhani wake
Muda wake kauuza kwa mwajiri
Nira kakabidhiwa
Mabega yote juu, meno yote nje
Ajisifu ana ajira!



Upendacho kukifanya, huthubutu kukifanya
Si wajua hakikupi muamala?
Usichopenda ndo' wakifanya kupata mkate wako
Kwa gharama ya muda wako mkate waupata
Muda huna shilingi wapata
Shilingi wapata kwa kumtumikia mwajiri
Na wadai u huru?

Saturday, July 2, 2011

CHANGAMOTO Insha za Jamii - Prof. Mbele



Natamani sana kukisoma kitabu hiki. Ninakitafuta kwa bidii. Unajua kinakopatikana?
Mwandishi Profesa Mbele anasema kakiandika kusahihisha majungu kuhusu Mwalimu Nyerere. Msome hapa halafu uone kama unaweza kujishindia Dola 100!

Waweza pia kusoma majadiliano katika Jamii Forums yanayodurusu ikiwa wanaomkosoa Mwalimu Nyerere wana hoja.

Friday, June 24, 2011

Take the Risk cha Ben Carson



Ndio kwanza nimeanza kukisoma. Take the Risk: learning to identify, Choose and Live with accepatable Risk. Kimeandikwa na Mganga Ben Carson kwa msaada wa Gregg Lewis na kuchapishwa na Zondervan Publishing House mwaka 2008.

Kitabu kinaanza na masimulizi ya upasuaji mgumu uliofanyika Julai 2003 kuwatenganisha Ladan na Laleh, mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana sehemu ya vichwa vyao. Mapacha hao hata hivyo walifariki dunia wakiwa na umri wa miaka 29 wakati upasuaji huo ukiendelea huko Singapore. Katika kitabu hiki, mwandishi anajaribu kutupatia somo lilitokana na Upasuaji huo.


Ladan na Laleh raia wa Iran muda mfupi kabla ya upasuaji huo uliofanyika Julai 2003.